JW subtitle extractor

Yakobo—Mwanamume Aliyependa Amani

Video Other languages Share text Share link Show times

Je, umewahi kukandamizwa
au kutendewa isivyo haki?
Umewahi kukasirishwa na jambo ambalo
mtu alisema au kutenda?
Sote tumepatwa na hali hiyo.
Katika hali kama hizo,
mara nyingi watu ambao hawamjui Yehova
wanapotendewa kwa njia hiyo hawatafuti amani.
Wanalipiza kisasi, wanapigana,
wanawashambulia wengine.
Lakini sisi tunajua kwamba Yehova anaona
jambo lililotokea, naye atarekebisha jambo hilo.
Ni jambo la hekima kukumbuka
maneno haya ya Yesu:
“Wenye furaha ni wale walio wapole.”
Wenye furaha ni wale wanaofanya amani.”
Biblia inamtaja mwanamume aliyedumisha
upole na amani katika hali ngumu sana
na zenye mkazo mwingi.
Tena na tena aliamua kwamba hatapigana
na badala yake akafanya amani na wengine.
Mwanamume huyo ni Yakobo.
Yakobo alijifunza kufanya amani kutoka kwa
mfano wa baba yake, Isaka.
Kulikuwa na njaa katika nchi hiyo,
na Isaka akahamishia familia yake huko Gerari
nchi iliyotawaliwa na Abimeleki
mfalme wa Wafilisti.
Acheni tusome kuhusu matatizo yaliyotokea
na jinsi Isaka alivyoyashughulikia.
Tafadhali fungua Mwanzo 26:12
Na Isaka akaanza kupanda mbegu
katika nchi hiyo,
na mwaka huo alivuna mara 100 zaidi
ya mbegu alizopanda,
kwa kuwa Yehova alikuwa akimbariki.
Mwanamume huyo akatajirika,
naye akaendelea kupata ufanisi
mpaka akawa tajiri sana.
Alipata makundi ya kondoo na
makundi ya ng’ombe
na kundi kubwa la watumishi,
nao Wafilisti wakaanza kumwonea wivu.
Kwa hiyo Wafilisti wakachukua udongo
na kuvifukia visima vyote ambavyo
watumishi wa baba yake walikuwa
wamechimba siku za Abrahamu.
Kisha Abimeleki akamwambia Isaka:
“Ondoka katika eneo letu,
kwa sababu umekuwa na
nguvu nyingi kuliko sisi.”
Kwa hiyo Isaka akaondoka huko
na kupiga kambi katika bonde la Gerari
na kuanza kuishi huko.
Na Isaka akavichimbua visima vilivyokuwa
vimechimbwa katika siku za Abrahamu baba
yake lakini ambavyo Wafilisti walivifukia baada
ya Abrahamu kufa, akavipa majina yaleyale
ambayo baba yake alivipa.
Watumishi wa Isaka walipokuwa wakichimba
bondeni, walipata kisima cha maji safi.
Nao wachungaji wa Gerari wakaanza
kugombana na wachungaji wa Isaka, wakisema:
“Maji haya ni yetu!”
Basi akakiita kisima hicho Eseki,
kwa sababu walikuwa wamegombana naye.
Nao wakaanza kuchimba kisima kingine,
wakaanza kukigombania pia.
Basi akakiita Sitna.
Baadaye akaondoka huko na
kuchimba kisima kingine,
lakini hawakukigombania.
Basi akakiita Rehobothi na kusema:
“Ni kwa sababu sasa Yehova ametupa nafasi ya
kutosha naye ametufanya tuongezeke nchini.”
Kisha akapanda kutoka huko
na kwenda Beer-sheba.
Yehova akamtokea usiku huo na kumwambia:
“Mimi ni Mungu wa Abrahamu baba yako.
Usiogope, kwa maana niko pamoja nawe,
nami nitakubariki na kufanya uzao wako
uwe mwingi kwa sababu
ya Abrahamu mtumishi wangu.”
Wafilisti wakichochewa na wivu wanafukia
visima ambavyo Abrahamu alikuwa amechimba.
Kisha mfalme anamwambia
Isaka aondoke katika eneo hilo.
Isaka anapaswa kufanya uamuzi,
labda watu fulani wanamwambia asiondoke.
Fikiria mambo ambayo huenda walimwambia:
“Hujafanya kosa lolote Isaka.
Yehova alikuambia kwamba wewe na
wazao wako mtaimiliki nchi hii.
Usiogope chochote.
Una watumishi wengi
na wana nguvu kuliko Wafilisti.
Una haki ya kulipiza kisasi dhidi ya
wale walioharibu visima vyako.”
Katika hali hiyo, wewe ungetendaje?
Isaka anaamua kudumisha amani,
anaamua kwamba ataondoka.
Hilo si jambo rahisi.
Isaka ana watumishi wengi,
pia ana idadi kubwa ya kondoo na ng’ombe.
Amelima mashamba, akapanda mbegu,
na kupata mazao mengi,
lakini anaacha mashamba hayo na kuondoka.
Lakini Isaka anakabili matatizo mengine zaidi.
Katika eneo analohamia, watumishi wake
wanachimba visima na wanapata maji safi.
Lakini wachungaji katika eneo hilo
wanasema: “Maji haya ni yetu!”
Kisha Isaka anachimba kisima kingine,
lakini wachungaji wa eneo hilo
wanagombania kisima hicho tena.
Tena, badala ya kupigania jambo hilo,
Isaka anahama na mwishowe anapata mahali
anapoweza kuishi kwa amani.
Yakobo aliona kwamba baba yake alipotenda
kwa amani alipata matokeo mazuri na alijua
kwamba Yehova alikuwa amembariki Isaka.
Tunapata somo gani?
Wazazi, msisahau kamwe kwamba
mfano wenu mzuri unaweza kuwa na
matokeo makubwa kwa watoto wenu.
Yakobo ana ndugu pacha, Esau.
Kati yao wawili,
Esau ndiye aliyezaliwa wa kwanza,
lakini Yehova anatabiri kwamba
tofauti na utamaduni,
Esau, mzaliwa wa kwanza,
angemtumikia ndugu yake mdogo.
Yehova anatambua mapema
sifa ambazo watasitawisha.
Na anajua kwamba Esau atakuwa mtu ambaye
hathamini mambo ya kiroho.
Hilo linakuwa wazi Esau anapobadilisha haki
yake ya kuwa mzaliwa wa kwanza
kwa bakuli la mchuzi,
na kukamilisha makubaliano hayo kwa kiapo.
Lakini mengi zaidi yanahusika,
anapouza haki yake ya mzaliwa wa kwanza,
pia anapoteza haki ya kupata baraka ya kinabii
kutoka kwa baba yake.
Miaka mingi inapita,
sasa Isaka amezeeka
anaamua kwamba ni wakati wa kumpa baraka
mzaliwa wake wa kwanza.
Huenda hajui kwamba tayari Esau ameuza
haki yake ya kuwa mzaliwa wa kwanza.
Vyovyote vile,
anamwambia Esau kwamba atambariki
lakini kwanza anamwambia amtayarishie
chakula kitamu, yaani,
mnyama wa mwituni aliyewindwa mbugani.
Rebeka, mama ya wale mapacha,
anasikia mazungumzo hayo
naye anamshawishi Yakobo ajifanye kwamba
yeye ni Esau ambaye
ameenda mbugani kuwinda.
Mpango huo unafanikiwa.
Bila kujua, Isaka anambariki Yakobo!
Esau anapotambua jambo hilo
anakasirika sana.
Acheni tusome simulizi hilo
kuanzia Mwanzo 27:41.
Hata hivyo,
Esau akawa na chuki kali dhidi ya Yakobo
kwa sababu ya baraka ambayo baba yake
alikuwa amempa,
na Esau akawa akisema moyoni mwake:
“Siku za kumwombolezea
baba yangu zinakaribia.
Zitakapokwisha nitamuua Yakobo ndugu yangu.”
Rebeka alipoambiwa maneno ya
Esau mwana wake mkubwa,
mara moja akaagiza Yakobo, mwana wake
mdogo aitwe, akamwambia: “Tazama!
Esau ndugu yako anapanga kukuua
ili kulipiza kisasi.
Sasa mwanangu, fanya ninayokwambia.
Ondoka,
ukimbilie kwa Labani ndugu yangu kule Harani.
Ishi naye kwa muda mpaka ghadhabu ya
ndugu yako itulie, mpaka hasira ambayo
ndugu yako anayo kukuelekea ipungue,
naye asahau mambo uliyomtendea.
Kisha nitatuma ujumbe ili urudi kutoka huko.
Kwa nini niwapoteze nyote wawili siku moja?”
Baada ya hayo
Rebeka akawa akimwambia Isaka:
“Ninachukia maisha yangu
kwa sababu ya mabinti wa Hethi.
Yakobo akioa mke kutoka kwa mabinti wa Hethi,
kama mabinti hawa wa nchi hii,
maisha yangu yana faida gani?”
Basi Isaka akamwita Yakobo,
akambariki na kumwamuru hivi:
“Usioe mke kutoka kwa mabinti wa Kanaani.
Nenda Padan-aramu katika nyumba ya Bethueli,
baba ya mama yako, na uoe mke kutoka kwa
mabinti wa Labani, ndugu ya mama yako.
Mungu Mweza-Yote atakubariki na kukufanya
uwe na wazao wengi na kuongezeka,
nawe hakika utakuwa kusanyiko la mataifa.
Naye atakupa wewe na uzao wako baraka
ambayo alimwahidi Abrahamu,
ili uimiliki nchi ambamo
umekuwa ukiishi kama mgeni,
nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu.”
Kwa hiyo Isaka akamruhusu Yakobo aondoke,
naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani
mwana wa Bethueli Mwaramu,
ndugu ya Rebeka, mama ya Yakobo na Esau.
Wazazi wa Yakobo wanamwambia afunge safari
kwenda kwa mjomba wake, Labani.
Bila shaka sababu kuu
ni tatizo kati yake na Esau.
Kumbuka kwamba hapo awali, kulikuwa na
mgogoro kati ya Isaka na Wafilisti,
tatizo ambalo inaonekana halikuweza
kutatuliwa kwa amani.
Basi, Isaka alifanya nini?
Alihamia sehemu nyingine.
Sasa Yakobo anakabili hali kama hiyo,
ndugu yake amewaka hasira,
basi Yakobo anaondoka.
Hilo linamaanisha kuondoka nyumbani
na kuacha familia yake;
kufunga safari ndefu kwenda nchi ya mbali.
Yakobo angeweza kuamua kwamba hataondoka
kwa sababu alimiliki haki ya mzaliwa wa kwanza.
Yakobo angeweza kubishana na wazazi wake
na kuwaambia:
‘Mimi si mtoto, nina umri wa miaka 77.’
Yakobo hakufanya hivyo.
Biblia inasema hivi:
“Yakobo alimtii baba yake na mama yake
na kwenda.”
Somo ni nini?
Tunapokabili hali ambayo haiwezi kutatuliwa
kwa amani, huenda tusihitaji kukimbia ili
kuokoa uhai wetu na kwenda nchi ya mbali.
Hata hivyo, wakati mwingine hali ya kutoelewana
inapotokea ni jambo la hekima kuondoka.
Methali 17:14 unasema:
“Kuanzisha vita ni kama
kufungua lango la mafuriko;
kabla ugomvi haujalipuka, ondoka.”
Yakobo akiwa njiani kwenda kwa mjomba wake,
Yehova anamtokea Yakobo katika ndoto na
kumhakikishia kwamba atamsaidia na kumlinda.
Hilo halimaanishi kwamba
matatizo ya Yakobo yamekwisha.
Mwishowe anawasili kwa mjomba wake
naye anaanza kuishi huko.
Baada ya muda,
hali nyingine inatokea ambayo inaonyesha
kwamba Yakobo ni mwanamume
anayependa amani.
Acheni tusome jambo hilo kuanzia
Mwanzo 29:16
Sasa Labani alikuwa na mabinti wawili.
Yule mkubwa aliitwa Lea,
na mdogo aliitwa Raheli.
Lakini macho ya Lea hayakuwa yaking’aa,
lakini Raheli alikuwa mwanamke mwenye
kuvutia sana, tena mrembo.
Yakobo alikuwa amempenda Raheli,
kwa hiyo akasema:
“Niko tayari kukutumikia kwa miaka saba
ili nimpate Raheli binti yako mdogo.”
Labani akasema:
“Ni afadhali nikupe wewe binti huyo
kuliko kumpa mwanamume mwingine.
Endelea kukaa nami.”
Basi Yakobo akamtumikia Labani kwa
miaka saba ili ampate Raheli,
lakini machoni pake miaka hiyo ilikuwa
kama siku chache tu kwa sababu ya
upendo aliokuwa nao kwa Raheli.
Kisha Yakobo akamwambia Labani:
“Nipe mke wangu nilale naye kwa sababu
siku zangu zimekwisha.”
Ndipo Labani akawakusanya wakaaji wote
wa eneo hilo na kufanya karamu.
Lakini wakati wa jioni,
akamchukua Lea binti yake na
kumleta kwa Yakobo ili alale naye.
Pia, Labani akamchukua Zilpa kijakazi wake
na kumpa Lea binti yake ili awe kijakazi wake.
Asubuhi Yakobo akagundua kwamba
alipewa Lea!
Kwa hiyo akamuuliza Labani:
“Ni jambo gani hili ulilonitendea?
Je, sikukutumikia ili nimpate Raheli?
Kwa nini umenitendea hila?”
Labani akamjibu:
“Si desturi yetu hapa kumwoza binti mdogo
kabla ya yule aliyezaliwa kwanza.
Sherehekea juma la mwanamke huyu.
Kisha utapewa mwanamke huyu mwingine
ukinitumikia kwa miaka mingine saba.”
Yakobo akafanya hivyo,
akasherehekea juma la mwanamke huyo,
kisha akampa Raheli binti yake awe mke wake.
Isitoshe, Labani alimchukua Bilha kijakazi wake
na kumpa Raheli binti yake ili awe kijakazi wake.
Yakobo ana sababu nzuri ya kukasirika.
Alikuwa amekubaliana na Labani kwamba
atafanya kazi miaka 7 ili kumpata Raheli.
Mwishoni mwa ile miaka 7,
karamu ya ndoa inapangwa lakini
mwanamke aliyefunikwa uso kabisa
ambaye analetwa si Raheli, ni Lea!
Hebu wazia jinsi Yakobo alivyoshtuka sana!
Badala ya kukubali kwamba ametenda kwa hila,
Labani anatoa visingizio.
Sasa Yakobo anafikiria nini?
Je, anafikiria kwamba huenda Yehova anatimiza
ahadi yake ya kumfanya Yakobo awe na wazao
wengi kama chembe za mavumbi ya ardhi?
Hatujui.
Na matokeo ni kwamba
Lea anamzalia wana 6, kutia ndani Lawi na Yuda
vichwa vya familia mbili ambazo
ziliheshimiwa zaidi kati ya makabila ya Israeli.
Bila shaka Yakobo hakujua hilo lingetokea.
Hata hivyo,
Yakobo mfanya amani anamkubali Lea
naye anakubaliana na ombi la Labani
la kushangaza kwamba afanye kazi
miaka 7 zaidi ili kumpata Raheli.
Somo ni nini?
Inavunja moyo sana wengine wanapokosa
kutimiza makubaliano.
Kama Yakobo,
je,
tunaweza kuwasamehe kutoka moyoni, na
kutafuta njia ya kudumisha amani pamoja nao?
Yakobo anamtumikia Labani kwa miaka 14
kwa ajili ya wake zake wawili
na anamfanyia Labani kazi kwa miaka mingine 6
ili kupata mifugo yake mwenyewe.
Mwishowe,
kwa mwongozo wa Yehova anakusanya familia
yake pamoja na mifugo yake na bila kumwambia
Labani anaanza safari ya kurudi nyumbani.
Labani anapotambua jambo hilo
anakasirika sana!
Anamfuatilia Yakobo na mwishowe anamfikia.
Hiyo ilikuwa hali hatari ambayo
ingeweza kusababisha vita.
Wazia jinsi ambavyo hali ingekuwa:
Yakobo alikuwa amefika kwenye eneo
lenye milima.
Labda ni asubuhi na hali ya hewa ni baridi.
Kuna sauti na harufu ya wanyama kondoo,
punda, ngamia, wanyama wengi.
Watumishi wanawatunza wanyama.
Wanawatayarisha kwa ajili ya safari ya siku hiyo.
Lakini ghafla wanaanza kupiga kelele kwa woga,
Labani amekuja na hayuko peke yake.
Anawasili pamoja na wanaume wenye nguvu.
Wanawasili wakiwa juu ya ngamia;
kisha wanashuka.
Hawa si wageni wenye urafiki.
Wanaume wa Labani wako tayari kutii
maagizo ya Labani.
Watumishi wa Yakobo wanakusanyika upesi
mahali hapo.
Kila mtu anamtazama Labani na Yakobo,
ambao wanabishana.
Usiku uliotangulia,
Yehova alikuwa amemwonya Labani
katika ndoto awe mwangalifu kuhusu mambo
atakayomwambia Yakobo.
Lakini bado Labani ana hasira na ugomvi.
Labani anamshtaki Yakobo kwa makosa mawili.
Kwanza, anasema:
“Kwa nini umenichezea akili,
na kwa kuwachukua mabinti wangu
kama mateka waliochukuliwa kwa upanga?
Kwa nini ulitoroka kwa siri, ukanichezea akili,
badala ya kuniambia?”
Jibu la shtaka hilo liko wazi.
Yakobo anajibu hivi:
“Ni kwa sababu niliogopa,
kwa maana nilisema moyoni mwangu, ‘Huenda
ukaninyang’anya kwa nguvu mabinti wako.’”
Labani pia anamshtaki Yakobo kwamba
amemwibia Miungu ya familia yake.
Ni kweli kwamba Raheli ameiba Miungu hiyo,
lakini Yakobo hajui lolote kuhusu hilo.
Wanafanya msako
lakini hawazipati sanamu hizo.
Kisha Yakobo anaanza kujitetea.
Acheni tuendelee na usomaji
kwenye Mwanzo 31:36.
Ndipo Yakobo akakasirika na kuanza
kumshutumu Labani.
Akamuuliza Labani:
“Nimefanya kosa gani,
nimetenda dhambi gani hivi kwamba
unanifuatia kwa bidii hivi?
Sasa kwa kuwa umepekua kabisa vitu vyangu
vyote, umepata nini cha nyumba yako?
Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu
na ndugu zako, waache waamue ni nani
mwenye kosa kati yetu.
Kwa miaka hii 20 ambayo nimekaa nawe,
mimba za kondoo wako na mbuzi wako
hazikuharibika, wala sijawahi kula
kondoo dume wa kundi lako.
Sijawahi kukuletea mnyama yeyote
aliyeraruliwa na mnyama wa mwituni.
Mimi mwenyewe nililipia hasara hiyo.
Ulidai malipo kutoka kwangu kwa ajili ya
mnyama yeyote aliyeibiwa mchana au usiku.
Jua lilinichoma wakati wa mchana na baridi
ilinipiga usiku, na macho yangu
yalipoteza usingizi.
Ilikuwa hivyo kwa miaka 20
niliyokaa nyumbani mwako.
Nimekutumikia kwa miaka 14
ili niwapate mabinti wako wawili
na kuchunga mifugo yako kwa miaka 6,
nawe ulibadili tena na tena
mshahara wangu mara kumi.
Ikiwa Mungu wa baba yangu,
Mungu wa Abrahamu,
Yule ambaye Isaka anamwogopa,
hangekuwa pamoja nami,
sasa ungeniambia niende zangu mikono mitupu.
Mungu ameyaona mateso yangu
na kazi ngumu ya mikono yangu, na ndiyo
sababu alikukaripia usiku wa kuamkia leo.”
Labani akamwambia Yakobo:
“Mabinti hawa ni mabinti wangu
na watoto hawa ni watoto wangu
na wanyama hawa ni wanyama wangu,
na kila kitu unachoona hapa
ni changu na cha mabinti wangu.
Ni jambo gani ninaloweza kufanya leo
kuwadhuru mabinti hawa au
kuwadhuru watoto wao ambao wamewazaa?
Sasa njoo, tufanye agano kati yetu,
wewe na mimi,
nalo litakuwa ushahidi kati yetu.”
Basi Yakobo akachukua jiwe
na kulisimamisha kama nguzo.
Kisha Yakobo akawaambia ndugu zake:
“Okoteni mawe!”
Basi wakaokota mawe na
kutengeneza rundo la mawe.
Halafu wakala chakula juu ya rundo
hilo la mawe.
Na Labani akaanza kuliita rundo hilo
Yegar-sahadutha,
lakini Yakobo akaliita Galeedi.
Ndipo Labani akasema:
“Rundo hili la mawe ni ushahidi kati yangu
mimi na wewe leo.”
Ndiyo sababu aliliita Galeedi,
na Mnara wa Mlinzi, kwa sababu alisema:
“Yehova na awe mlinzi kati yangu mimi
na wewe tunapokuwa hatuonani.
Ukiwatesa mabinti wangu
na kuanza kuoa wake wengine
kuongezea mabinti wangu,
hata mwanadamu asipoona jambo hilo,
kumbuka kwamba Mungu atakuwa
shahidi kati yangu mimi na wewe.”
Labani akaendelea kumwambia Yakobo:
“Hili hapa ni rundo la mawe,
na hii hapa ni nguzo ambayo nimesimamisha
kati yangu mimi na wewe.
Rundo hili la mawe ni ushahidi,
na nguzo hii pia ni ushahidi kwamba
sitapita rundo hili la mawe ili kuja kukudhuru,
nawe hutapita rundo hili la mawe
na nguzo hii ili kuja kunidhuru.
Mungu wa Abrahamu na Mungu wa Nahori,
Mungu wa baba yao,
na awe mwamuzi kati yetu.”
Basi Yakobo akaapa kwa jina la Yule
ambaye Isaka baba yake alimwogopa.
Kisha Yakobo akatoa dhabihu mlimani na
kuwaalika ndugu zake wale chakula.
Wakala na kulala mlimani usiku huo.
Hata hivyo,
Labani akaamka asubuhi na mapema,
akawabusu wajukuu wake na mabinti zake
na kuwabariki.
Kisha Labani akaondoka, akarudi nyumbani.
Yakobo alikuwa amemtumikia Labani
kwa uaminifu kwa miaka 20,
ingawa Labani alikuwa amemdanganya
na kumdhulumu.
Labani hakubaliani na jambo hilo,
badala yake kwa udanganyifu anadai kwamba
yeye ndiye mmiliki halali wa Yakobo
na kila kitu alicho nacho.
Kisha Labani anapendekeza kwamba
wafanye agano la amani ili kuhakikisha kwamba
familia moja haitaidhuru familia nyingine.
Pendekezo la Labani halichochewi na
nia ya kufanya amani.
Labda alitaka kuhakikisha kwamba Yakobo
hatarudi na ile miungu ya familia baada ya kifo
cha Labani na kuwanyang’anya wanawe urithi.
Vyovyote vile, Yakobo anakubaliana naye;
kila mtu anatulia; hakutakuwa na vita.
Kisha wanajenga mnara ili kukumbuka
makubaliano hayo.
Licha ya kukandamizwa kwa miaka mingi,
Yakobo anakubali kufanya agano la amani.
Anaamua kutoweka kinyongo
wala kulipiza kisasi.
Yakobo anafaulu kushinda changamoto hiyo.
Lakini sasa atakabili changamoto nyingine.
Yakobo anawatuma wajumbe kwa ndugu yake.
Wanamwambia kwamba Yakobo anarudi
naye anaomba kupata kibali cha Esau.
Wajumbe hao wanarudi na habari kwamba
Esau yuko njiani kuja kukutana na Yakobo
na pamoja naye ana wanaume 400.
Jamani je, bado Esau ana hasira?
Inaeleweka kwamba Yakobo ana wasiwasi.
Hataki kupigana na ndugu yake.
Acheni tuone jinsi alivyoshughulikia hali hiyo.
Tafadhali fungua Mwanzo 32:13
Naye Yakobo akalala huko usiku huo.
Kisha akachukua baadhi ya mali zake
ili ampe zawadi Esau ndugu yake:
mbuzi jike 200, mbuzi dume 20, kondoo jike 200,
kondoo dume 20, ngamia 30 wanaonyonyesha,
ng’ombe 40, ng’ombe dume 10, punda jike 20,
na punda dume 10 waliokomaa.
Akawapa watumishi wake kundi moja
baada ya lingine, akawaambia:
“Nitangulieni mvuke kabla yangu,
nanyi mwache nafasi kati ya kundi moja
na kundi lingine.”
Pia akamwamuru hivi yule wa kwanza:
“Ikiwa Esau ndugu yangu atakutana nawe
na kukuuliza, ‘Wewe ni mtumishi wa nani,
unaenda wapi, na wanyama hawa walio
mbele yako ni wa nani?’ utamwambia,
‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo.
Ni zawadi aliyokutumia wewe,
bwana wangu Esau, na tazama!
yeye mwenyewe yuko nyuma anatufuata.’”
Akamwamuru hivi pia mtumishi wa pili,
wa tatu, na wale wote waliokuwa wakiyafuata
makundi hayo: “Mkikutana na Esau,
mtamwambia maneno hayohayo.
Vilevile mtamwambia,
‘Mtumishi wako Yakobo
yuko nyuma anatufuata.’”
Kwa maana Yakobo alisema moyoni mwake:
‘Nikimtumia zawadi kwanza huenda nikamtuliza,
na huenda atanipokea kwa fadhili
nitakapokutana naye baadaye.’
Yakobo anataka kuwa na amani pamoja
na ndugu yake.
Anatuma zawadi kubwa, mamia ya wanyama
ili kufanya hilo liwezekane.
Je, hilo linamaanisha kwamba
Yakobo alikuwa dhaifu, na kwamba
anaogopa kukutana na ndugu yake?
Hapana!
Kumbuka, kabla ya kukutana na Esau,
Yakobo anapigana mweleka na malaika
mpaka kunapopambazuka
Ili kupata uhakikisho zaidi kwamba
Yehova atambariki.
Acheni sasa tuone jambo linalotokea
ndugu hao wawili wanapokutana.
Tafadhali fungua Mwanzo 33:1.
Sasa Yakobo akainua macho yake
na kumwona Esau akija
pamoja na wanaume 400.
Kwa hiyo akawagawa watoto kati ya Lea,
Raheli, na wale vijakazi wawili.
Akawaweka vijakazi na watoto wao mbele,
kisha Lea na watoto wake,
halafu Raheli na Yosefu nyuma yao.
Kisha yeye mwenyewe akaenda mbele yao,
akainama mpaka chini mara saba huku
akimkaribia ndugu yake.
Lakini Esau akakimbia kukutana naye,
akamkumbatia na kumbusu,
nao wakatokwa na machozi.
Alipoinua macho yake na kuona wanawake
na watoto, akauliza:
“Ni nani hawa walio pamoja nawe?”
Yakobo akamwambia:
“Ni watoto ambao Mungu amenipa
kwa fadhili mimi mtumishi wako.”
Ndipo wale vijakazi wakaja mbele na watoto wao
na kuinama chini, Lea pia akaja mbele
na watoto wake, nao wakainama chini.
Kisha Yosefu akaja mbele na Raheli,
nao wakainama chini.
Esau akauliza: “Msafara huu wote ni wa nini?”
Yakobo akamjibu:
“Nimekuja ili kupata kibali machoni pako,
bwana wangu.”
Esau akasema:
“Nina mali nyingi sana, ndugu yangu.
Usinipe mali zako.”
Lakini Yakobo akasema:
“Hapana, tafadhali nakusihi.
Ikiwa nimepata kibali machoni pako,
pokea zawadi yangu kutoka mkononi mwangu,
kwa sababu nimekuletea ili niuone uso wako.
Nami nimeona uso wako kana kwamba
nimeona uso wa Mungu,
kwa maana umenipokea kwa furaha.
Tafadhali pokea zawadi yangu ya baraka
uliyoletewa, kwa sababu Mungu amenibariki,
nami nina kila kitu ninachohitaji.”
Basi akaendelea kumsihi apokee zawadi hiyo,
naye akaichukua.
Hayo yalikuwa matokeo mazuri!
Badala ya kukutana kwa hasira,
wanaungana tena kwa shangwe.
Wanaume hao wawili wanalia na kukumbatiana.
Kwa mara nyingine tena,
Yakobo anafanya amani.
Alifanyaje hivyo?
Alisali kisha akatenda kupatana na sala zake.
Alituma zawadi.
Alimwonyesha ndugu yake staha na heshima
akamwita bwana na kuinama mbele zake
mara saba.
Somo ni nini?
Simulizi hili linaonyesha vizuri kwamba
tunapaswa kufanya yote tuwezayo ili kudumisha
amani pamoja na ndugu na dada zetu Wakristo.
Tumejifunza mengi sana kutoka kwa
Yakobo kuhusu kufanya amani.
Ndugu yake alipotishia kumuua
walipokuwa nyumbani, aliamua kuondoka.
Labani alipomdanganya kuhusu Raheli na Lea,
alikubaliana na Labani.
Labani alipomfuatilia na
na kumtolea mashtaka Yakobo,
alikubali kufanya agano la amani.
Na alipokuwa karibu kukutana na Esau,
alituma zawadi.
Kumbuka kwamba katika visa hivyo vyote,
Yakobo hakuhitaji kuomba msamaha.
Lakini katika maisha yake yote,
Yakobo alipenda amani.
Alimtegemea Yehova, na Yehova akambariki.
Yehova hakumsahau kamwe Yakobo
na jinsi alivyojitahidi kufanya amani
aliposhughulika na wengine.
Tunapofanya hivyo pia,
yaani, tukijitahidi kufanya amani,
licha ya kutendewa isivyo haki,
tunapokabili mateso,
katika mambo madogo na pia mambo makubwa,
Yehova hatatusahau pia.
Yehova atatubariki sana ikiwa tutapenda amani,
kama vile Yakobo alivyopenda amani.